MFUKO WA MAFAO YA KUSTAAFU
RETIREMENT BENEFITS FUND
Menu

Mpango Wa Hiari Wa Kujiwekea Akiba Uzeeni "VSRS"

Mpango wa kujiwekea akiba ya uzeeni (VSRS) ulianzishwa na Mfuko mnamo mwaka 2009 kwa lengo la kuwawezesha watu wote wenye uwezo wa kuzalisha kipato kujiwekea akiba ili kuwasaidia kutimiza malengo yao katika maisha kama vile kuanzisha au kukuza biashara, matibabu, ujenzi, kulipa ada za shule na kukabiliana na majanga mbali mbali, hasa pale uwezo au nguvu ya kuzalisha kipato inapopungua. Majanga yapo ya aina nyingi kama vile moto, mafuriko, ukame, ajali na magonjwa mbali mbali yanayosababisha binadamu asiweze kukabiliana nayo kwa haraka pindi yanapotokea.
 

Nani anaweza kuwa Mwanachama wa Mpango wa Hiari?

Mtu yeyote mwenye uwezo wa kuzalisha kipato anaweza kujiunga na mpango huu, awe ameajiriwa na anachangia kwenye Mfuko wowote wa Hifadhi ya jamii au amejiajiri mwenyewe kama vile;

·         Mkulima  

·         Mvuvi 

·         Mama Lishe                

·         Dereva boda boda       

·         Mjasiriamali yoyote
 

Mgawanyo wa wanachama wa Mpango wa Hiari

 

Gharama ya kujiunga na Mpango wa Hiari wa kujiwekea Akiba ya Uzeeni
Kujiunga na Mpango huu ni Bure
 

Kiwango cha uchangiaji na muda wa kujiwekea Akiba

Kiwango chochote kinaruhusiwa kuanza kujiwekea akiba kulingana na uwezo wa mwanachama. Mwanachama anaweza kuweka akiba wakati wowote, iwe kila siku, kila wiki, kila mwezi au kwa msimu.
 

Mwanachama anaweza kujiwekea akiba kwa njia zifuatazo:

 • Simu ya Kiganjani (M-pesa, Tigo pesa au Airtel Money)
 • Benki kama vile CRDB, NMB, NBC au benki yoyote mwanachama anakotunza fedha zake.
 • Mawakala waliothibitishwa na GEPF
 • Kuwasilisha moja kwa  moja kwenye Ofisi za Mfuko wa GEPF zilizo Mikoani au Makao Makuu.
   

Riba Kwa Wanachama

Wanachama wa mpango wa hiari wa kujiwekea akiba hulipwa riba kutokana na michango yao. Wengi wa wanachama hawa hawakidhi vigezo vya kulipwa pensheni hivyo wanasalia katika utaratibu wa akiba.  Pamoja na wanachama wa mpango wa hiari kuna baadhi ya wanachama walioko katika mpango wa lazima ambao hawatakidhi kulipwa pensheni hivyo nao pia watalipwa michango yao pamoja na riba. Kwa sasa Mfuko unatoa riba ya 7.5%. Kiasi hiki kinatolewa ili kulinda thamani ya michango ya wanachama.
 

Faida za kujiunga na Mpango wa Hiari wa kujiwekea Akiba ya Uzeeni

 • Hakuna gharama yoyote inayotozwa wakati wa kuweka akiba.
 • Gawio kubwa la mapato linaloongezeka kila mwaka linalotokana na uwekezaji kwenye vitega uchumi mbali mbali.
 • Mwanachama anaweza kuchukua sehemu ya akiba yake wakati wowote wa dharura bila kutozwa fedha yoyote.
 • Kupata malipo bila usumbufu ndani ya siku saba za kazi.
 • Michango ya mwanachama inamuwezesha kulipwa pensheni endapo ataweka kiasi na muda unaofuzu vigezo vya kulipwa pensheni.
 • Mikopo kupitia SACCOS au vikundi vilivyojisajili vya wanachama.
 • Kupatiwa pembejeo za kilimo kwa wakulima wanaozalisha kwa wingi.
   

Njia za ulipaji Mafao kwa Mwanachama

 • Malipo ya moja kwa moja kwenye Akaunti ya Benki ya mwanachama
 • Malipo kwa kutumia Hundi
 • Malipo ya papo hapo ya fedha taslimu kwa kiwango kilichoidhinishwa na Bodi ya Wadhamini ya Mfuko.